Rais wa Marekani, Donald Trump muda mfupi uliopita alimpokea mwenzake wa China, Xi Jinping jijini Washington, hili likiwa ni tukio la kipekee kwa Trump kumpokea mwenyerwe mgeni wake katika uwanja wa ndege.
Ziara ya XI Jinping inakuja ikiwa imepita miezi minne tangu Trump azuru Beijing katika ziara iliyolenga kujaribu kumaliza tofauti baina ya mataifa hayo mawili yenye nguvu duniani.
Akiwa China, Rais Trump alimualika mwenzake kwa ziara kama hiyo, ambapo ajenda kubwa ya Beijing na Washington ni kuhusu mvutano wa kibiashara, usalama na ushirikiano wa masuala yenye tija kwa nchi hizo.
Vyombo vya habari vya Serikali ya China vimeripoti kuwa rais Xi Jinping anataka nchi hizo mbili ziwe washirika badala ya kuwa maadui, kauli inayoonesha utayari wa Beijing kurekebisha uhusiano ulioanza kudorora kati yake na Washington.
Kufuatia ziara hii, waziri wa biashara wa Marekani alitangaza kuongezwa muda wa mazungumzo ya kibiashara baina ya nchi zao, hatua ambayo pengine itatoa nafasi kwa rais Trump na Xi, kukubaliana namna bora zaidi ya kufanya biashara bila kuchukuliana hatua za kulipizana kisasi.
Xi atafanya ziara ya siku 3 kwenye taifa hilo, ambapo Trump anatarajiwa kumgusia kuhusu raia wake waliofungwa kwenye jela za China, pamoja na kuitaka iache uungaji mkono wake kwa utawala wa Tehran.