Waasi wa Houthi nchini Yemen wameituhumu Saudi Arabia kwa kutekeleza shambulio la anga kwenye gereza kaskazini mwa Mji wa al-Hazm, shambulio ambalo lilisbaabisha vifo vya watu saba akiwemo mtoto.
Karibia watu wengine saba walijeruhiwa kwenye shambulio hilo kwenye gereza hilo nchini Yemen kwenye mpaka na Saudi Arabia kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya afya inayoongozwa na waasi wa Houthi.
Televisheni ya Al Masirah inayosimamiwa na Houthi, ilionyesha picha ilizosema ni za baada ya shambulio hilo, ikiwemo jengo ambalo liliharibiwa kwenye shambulio hilo.
Hadi tukichapisha taarifa hii, Saudi Arabia haikuwa imezungumzia madai ya Houthi.
Televisheni ya Al Masirah pia ilichapisha video iliodai ni ya waasi wa Houthi wakiishambulia malori ya Saudi Arabia yaliokuwa yamebeba vifaa vya kijeshi.
Msemaji wa Houthi Yahya Saree ameituhumu Saudi Arabia kwa kutekeleza mauaji ya halaiki katika Mji wa al-Jawf.
Madai ya Houthi yamejiri wakati huu makabiliano yakiripotiwa kati ya kundi hilo lenye silaha na serikali ya Yemen inayotambuliwa kimataifa katika siku za hivi karibuni.