Waziri Mkuu mpya wa Ufaransa Sebastien Lecornu ajiuzulu

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amekubali hatua ya Waziri wake Mkuu Sebastien Lecornu kutangaza kujiuzulu saa chache baada ya kulitaja baraza lake la Mawaziri kulingana na taarifa kutoka kwa Ofisi ya Rais.

Kulingana na wachambuzi wa kisiasa, hatua hii inalitumbukiza zaidi taifa hilo la Ulaya kwenye mkwamo wa kisiasa.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alimteua Lecornu, Waziri wa zamani wa ulinzi kwenye wadhifa huo mwezi uliopita.

Baraza jipya la Mawaziri ambalo Macron alitangaza Jumapili ya wiki iliopita kufanya kazi na Lecornu limepingwa kisiasa, baadhi ya wapinzani wake wakiwa na maoni mseto kulihusu.

Lecornu alikuwa anakabiliwa na kibarua kigumu cha kuja na bajeti ya mwaka ujao, itakayokubaliwa na bunge.

Watangulizi wa Lecornu, Francois Bayrou na Michel Barnier, waliondolewa madarakani na wabunge kutokana na mvutano kuhusu matumizi ya serikali na kubana matumizi.

Takwimu rasimi zinaonyesha kwamba deni la taifa la Ufaransa limekuwa kubwa zaidi.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii