Jamii imetakiwa kushiriki kikamilifu katika kukomesha vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia kwa kutoa taarifa na ushahidi mahakamani pale inapohitajika kufanya hivyo.
Rai hiyo imetolewa na ASP Pili Saburi, Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto kutoka Jeshi la Polisi Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, alipokuwa akizungumza katika kipindi cha Sega la Leo.
Kipindi hicho kilitoa elimu kuhusu nafasi ya mwalimu katika kumsaidia mtoto aliyefanyiwa ukatili wa kingono, kihisia, maneno au unyanyasaji ndani ya mazingira ya shule.
ASP Saburi amesema kuwa ili kesi za ukatili wa kijinsia zifanikiwe, ni lazima kuwe na ushirikiano wa karibu kati ya mpelelezi, mtoa ushahidi, daktari pamoja na jaji au hakimu, ili kuhakikisha haki inatendeka na sheria inachukua mkondo wake dhidi ya mtuhumiwa.
Aidha, amewataka wazazi, walezi, walimu na jamii kwa ujumla kuwajengea uwezo watoto wa kujiamini na kujisemea wanapofanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Amesisitiza kuwa makosa kama kubaka, kulawiti na kupiga ni makosa ya jinai yanayoadhibiwa kwa kifungo cha kuanzia miaka 15 jela hadi kifungo cha maisha.
ASP Saburi amesisitiza umuhimu wa elimu endelevu kwa jamii ili kupunguza matukio ya ukatili na kuhakikisha watoto wanalelewa katika mazingira salama na yenye kulindwa kisheria.
Sasa ili kupata undani wa taarifa hii tafadhali usikose kutufuatilie na Usikilize jembe Habari Kamili hapo saa saba kamili mchana ambapo msomaji wetu wa hii leo ni Evance Mlyakado tafadhali usipitwe na taarifa zetu Mahiri kabisa.
Lakini pia tembelea mitandao yetu ya kijamii ya Jembefmtz
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime