Wananchi wa Mtaa wa Nyanza, Kata ya Kalangalala, Halmashauri ya Manispaa ya Geita mkoani Geita, wamelalamikia usumbufu unaodaiwa kusababishwa na shughuli za mwekezaji Lespio Gold Mine zinazofanyika usiku na mchana katika eneo hilo.
Malalamiko hayo yametolewa Februari 16, 2026 mbele ya Diwani wa Kata hiyo, Reuben Sagayika, katika mkutano wa hadhara uliofanyika mtaani hapo.
Wananchi wameeleza kuwa shughuli za upasuaji miamba pamoja na kelele za mitambo zimekuwa zikisababisha usumbufu mkubwa na kuathiri maisha yao ya kila siku.
Akizungumzia sakata hilo Mhandisi wa Migodi kutoka Ofisi ya RMO Mkoa wa Geita, Bw. John Ayoub, amesema kuwa kwa sasa shughuli za upasuaji miamba zimesitishwa hadi taratibu za tathmini zitakapofanyika upya sambamba na ulipaji wa fidia kwa wananchi wanaoathirika.
Kwa upande wake, Meneja wa kampuni hiyo, Bw. Soud Mtafuni amesema wamepokea maelekezo ya serikali na tayari wameanza mchakato wa kulipa fidia, akiahidi kuwa hatua hizo zitakamilishwa kwa haraka ili kuruhusu shughuli kuendelea bila kuathiri wananchi.
Naye Diwani wa Kata ya Kalangalala, Reuben Sagayika, amewataka wananchi kuwa watulivu huku akisisitiza kuwa suala hilo litashughulikiwa kwa kuzingatia maslahi ya pande zote.
Sasa ili kupata undani wa taarifa hii tafadhali usikose kutufuatilie na Usikilize jembe Habari Kamili hapo saa kumi kamili jioni ambapo msomaji wetu wa hii leo ni Evance Mlyakado tafadhali usipitwe na taarifa zetu Mahiri kabisa.
Lakini pia tembelea mitandao yetu ya kijamii ya Jembefmtz
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime