Hofu Yatawala Bariadi Kufuatia Maji Machafu ya Kiwanda

Hali ya wasiwasi na hofu imetanda kwa wakazi wa Kata ya Isanga, Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu kufuatia madai ya kiwanda cha kuchakata pamba na alizeti kutiririsha maji machafu yanayodaiwa kuwa na kemikali hatarishi.

Baadhi ya wananchi wameeleza kuwa maji hayo yamekuwa yakitiririka katika maeneo ya makazi na mashamba, hali inayodaiwa kuathiri mifugo, mazao pamoja na mazingira kwa ujumla.

Wameiomba Serikali kuingilia kati haraka ili kuzuia madhara zaidi yanayoweza kujitokeza.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Katenga, Sitta Masunga, pamoja na Diwani wa Kata ya Isanga Nashoni Ngusa wamesema tayari athari zimeanza kuonekana wakisisitiza umuhimu wa mamlaka husika kuchukua hatua za haraka kulinda afya za wananchi na mali zao.

Kwa upande wake Afisa Mazingira wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi Monica Deusdedith amesema ofisi yake imeanza kufuatilia suala hilo na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya uongozi wa kiwanda hicho.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi Nkenyenge Charles Nkenyenge ameahidi kuwa halmashauri haitavumilia vitendo vinavyohatarisha mazingira na afya za wananchi akibainisha kuwa hatua stahiki zitaendelea kuchukuliwa ili kukomesha tatizo hilo.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii