Sheikh Kabeke Azitaka Kamati za Mwezi Kanda ya Ziwa Kutoa Taarifa Sahihi za Ramadhani

Sheikh wa Mkoa wa Mwanza na Mjumbe wa Kamati ya Mwezi Kitaifa anayewakilisha Kanda ya Ziwa, Sheikh Hasan Kabeke, amezitaka kamati za mwezi katika mikoa yote ya Kanda ya Ziwa kutoa taarifa sahihi mara tu watakapouona muandamo wa mwezi wa Ramadhani.

Akizungumza leo katika ofisi za BAKWATA Mkoa wa Mwanza, Sheikh Kabeke amesema ni wajibu wa kamati za mwezi kuanzia ngazi ya kata, wilaya hadi mkoa kuhakikisha wanautazama kwa umakini muandamo huo ili kuwahakikishia Waislamu wanapata taarifa sahihi na kwa wakati kuhusu kuanza kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Amesisitiza kuwa utoaji wa taarifa kwa wakati utasaidia kuepusha mkanganyiko na kuimarisha umoja miongoni mwa waumini katika Kanda ya Ziwa.

Aidha, amewataka Waislamu kuwa watulivu katika kipindi hiki cha kusubiri muandamo wa mwezi na kuwasikiliza viongozi wao wa dini katika ngazi zote ili kufuata mwongozo rasmi utakapotolewa.

Waislamu kote nchini wanatarajiwa kuanza ibada ya kufunga mara baada ya kuthibitishwa kuandama kwa mwezi wa Ramadhani, ambao ni nguzo ya nne ya Uislamu, unaowataka waumini kufunga kwa siku 29 au 30.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii