Serikali ya Lebanon imetangaza kuwa jeshi lake litahitaji angalau miezi minne kuanza awamu ya pili ya mpango wa kuwapokonya silaha wanamgambo wa kundi la Hezbollah kusini mwa nchi hiyo.
Mpango huo ulianzishwa mwaka 2025 baada ya Hezbollah kudhoofika kufuatia vita vyake na Israel, ambapo jukumu la utekelezaji lilikabidhiwa kwa Jeshi la Lebanon.
Mwezi Januari 2026, jeshi lilitangaza kukamilika kwa awamu ya kwanza ya operesheni hiyo, iliyohusisha eneo kati ya Mto Litani na mpaka wa Israel.
Awamu ya pili inatarajiwa kuhusisha eneo kati ya mito Litani na Awali, umbali wa takribani kilomita 40 kusini mwa mji mkuu Beirut.
Hata hivyo, Israel imekuwa ikikosoa juhudi za jeshi la Lebanon, ikidai hazitoshi kwani Hezbollah inaendelea kujiimarisha.
Kutokana na hali hiyo Israel imeendeleza mashambulizi ya mara kwa mara nchini Lebanon licha ya makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa mwezi Novemba 2024.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime