Mgodi wa Dhahabu wa Geita Gold Mining Limited (GGML), kupitia mpango wake wa Kilimanjaro Challenge Against HIV and AIDS Trust (Kili Trust), umeandaa warsha maalum ya kuwajengea uwezo wanufaika wake itakayofanyika jijini Mwanza kuanzia Februari 16 hadi 20, 2026.
Warsha hiyo itawakutanisha wanufaika, wadau wa utekelezaji, washirika na wadhamini kwa lengo la kuimarisha utawala bora, uwajibikaji wa kifedha na kuongeza matokeo chanya ya programu.
Hatua hiyo ni sehemu muhimu ya maandalizi kabla ya utoaji wa fedha kupitia Kili Grants Portfolio ya mwaka 2024/2025, inayolenga kusaidia miradi ya uwezeshaji wa kiuchumi, uimarishaji wa afya za jamii na mipango endelevu.
Kupitia mpango huo, jumla ya watu 2,309 wananufaika moja kwa moja na wengine 19,690 kwa njia isiyo ya moja kwa moja katika mikoa sita ya Tanzania.
Kili Trust imezitaka taasisi zitakazonufaika kupitia mchakato wa uhakiki wa kina (due diligence), mafunzo elekezi kabla ya utekelezaji wa miradi, pamoja na mafunzo ya usimamizi wa ruzuku, fedha na ufuatiliaji na tathmini, kabla ya kupokea fedha.
Lengo ni kuhakikisha matumizi ya fedha yanafanyika kwa uwazi, ufanisi na kwa kuzingatia malengo yaliyokusudiwa.
Akizungumza katika warsha hiyo, Meneja wa Kili Trust, Bw. Stephen Mhando, amesema Kili Challenge si tukio la kuchangisha fedha pekee, bali ni wito wa kitaifa unaowaunganisha washirika, jamii na watu binafsi kusimama pamoja na watu wanaoishi na VVU na UKIMWI.
Amesema kupitia rasilimali zinazokusanywa kila mwaka, Trust inaendelea kupanua afua zenye kuleta mabadiliko chanya, ikiwemo uwezeshaji wa kiuchumi, kuboresha upatikanaji wa huduma za afya na kupunguza unyanyapaa, ili kuhakikisha matokeo endelevu katika jamii.
Mwaka huu, programu imepanua wigo kwa kuwajumuisha wachimbaji wadogo kama kundi lenye hatari zaidi ya maambukizi ya VVU kutokana na uhamahama, mazingira yasiyo rasmi ya kazi na upatikanaji mdogo wa huduma za afya.
Afua zitajikita katika kuongeza uelewa, kuimarisha kinga, upimaji, uunganishaji wa matibabu na kujenga ustahimilivu wa jamii katika maeneo ya uchimbaji.
Kili Challenge inaendelea kufadhili afua mbalimbali zikiwemo uwezeshaji wa kiuchumi kwa watu wanaoishi na VVU, mipango ya usalama wa chakula, huduma za kinga na matibabu katika jamii, kupunguza unyanyapaa, msaada wa kisaikolojia, pamoja na kuimarisha mifumo ya afya na mitandao ya rufaa.
Wakati maandalizi ya Kili Challenge 2026 yakishika kasi, Trust imezihimiza kampuni, taasisi na watu binafsi kushiriki katika kampeni ya mwaka huu kwa lengo la kuchangisha dola za Marekani milioni 1 ifikapo 2026, ili kuendeleza azma ya Tanzania na UNAIDS ya kutokomeza janga la UKIMWI ifikapo mwaka 2030.
Kili Challenge ilianzishwa mwaka 2002 na GGML na imekuwa miongoni mwa mipango mikubwa ya sekta binafsi nchini katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI, kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS).
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime